
Dk. John Magufuli na mgombea mwenza, Samia Suluhu Hassan, wakiwasalimia wakazi wa Jiji la Dar es Salaam jana.
Mgombe uraiswa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John
Pombe Magufuli jana alichukua fomu za kuwania nafasi hiyo huku Mwenyeti
wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, akiwaasa wanachama wa chama hicho
wasimpuuze adui yeyote katika uchaguzi mkuu mwaka huu na kutamba
watafunga magori uwanjani huku wapinzani wakiwatazama.
Magufuli alichukua fomu hizo katika ofisi za Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (Nec) kwa mbwembwe akiwa kwenye msafara wa magari, pikipiki,
matarumbeta na muziki.
Akizungumza na wanachama wa CCM jana mchana katika ofisi ndogo za
chama hicho zilizopo mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam, Rais Kikwete
aliwasihi wanachama wa chama hicho kutodharau adui yeyote watayepambana
naye katika uchaguzi mkuu mwaka huu.
Licha ya Rais Kikwete kutofafanua kauli yake hiyo, katika uchaguzi
mkuu ujao CCM inatarajia kupambana vikali na mgombea urais kupitia
Ukawa, Edward Lowassa aliyehama Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) hivi karibuni.
Lowassa alikihama CCM huku akisema kwamba ameamua kufanya hivyo
kutokana na kubakwa kwa demokrasia ndani ya chama hicho kikongwe nchini.
Kikwete alisema katika uchaguzi wa mwaka huu, chama hicho kitafunga
magori uwanjani huku upinzani ukitazama na kwamba kitapata ushindi wa
kishindo na hilo hana wasiwasi nalo.
Rais Kikwete jana alionekana mwenye furaha muda wote huku akiomba
kikundi cha kwaya cha TOT, kimuwekea wimbo wa 'acha waseme CCM kina
wenyewe, shangilia ushindi unakuja'.
Wakati wimbo huo ukipigwa, Kikwete aliamua kuucheza akiwa jukwaani
huku akishangiliwa na wananchi waliokusanyika katika ofisi za CCM.
Hata hivyo, Rais Kikwete hakuzungumzia juu ya kuondoka Lowassa
ndani ya CCM, na kwenda kujiunga na Chadema kisha kuteuliwa kugombea
urais kupitia umoja huo.
Alisema dunia nzima inajua maendeleo mazuri yaliyofikiwa kupitia
utawala wake na kwamba katika kampeni watakwenda kuwaeleza wananchi
mambo mazuri yaliyofanywa.
Alijivunia maendeleo makubwa yaliyopatikana katika utawala wake na
kusisitiza kuwa anaondoka madarakani huku akiiacha nchi ikiwa na amani,
umoja na mshikamano.
Wakati wa kwenda kuchukua fomu ya kugombea urais, Dk. Magufuli jana
aliambatana na mgombea mwenza, Samia Suluhu Hassan kwenye Ofisi za
Makao Makuu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), huku wakisindikizwa na
viongozi mbalimbali waandamizi wa CCM.
Wengine ni wajumbe wa kamati kuu za CCM, baadhi ya mawaziri, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecki Sadiki.
Tukio hilo lilisababisha shughuli za mbalimbali za wananchi
kusimama kwa muda kupisha msafara huo kupita wakati ukitokea Nec
kuelekea ofisi za CCM kabla ya kuhutubiwa na wagombea na viongozi wa
chama hicho.
Mgombea huyo alichukua fomu jana mchana katika ofisi ya Nec kisha
msafara wake ambao ulifunga barabara za Bibi Titi Mohammed, Morogoro na
Ohio, ulirudi ofisi ndogo za CCM zilizopo Mtaa wa Lumumba ambako
aliwahutubia wanachama na wapenzi wa chama hicho.
KINANA
Akimkaribisha Rais Kikwete kuwatuhutubia wanachama hao na wapenzi
wa CCM, Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdurlahman Kinana, alitoa maneno
makali huku akidai wanachama waliohamia upinzani kuwa ni makapi.
Kinana alidai CCM hakiwezi kupambana na makapi katika uchaguzi huo
wa madiwani, wabunge na rais huku akisisitiza kuwa ushindi ni lazima
upatikane kwa chama hicho Oktoba 25, mwaka huu.
MAGUFULI
Kwa upande wake , Dk. Magufuli ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi,
alisema shida zote za Watanzania anazifahamu na mategemeo yao
anayafahamu na kuendelea kuwaahidi kwamba hawaangusha wakimpa nafasi ya
kuwa rais wa serikali ya awamu ya tano.
Alisema serikali ya awamu ya nne imefanya mambo mengi yakiwamo ya
ujenzi wa barabara ambazo pia wapinzani wanazitumia kupita, hivyo
akishinda, ataziendeleza.
"Mnitume nitakuwa mtumishi wenu mzuri kwa kuwa shida za Watanzania
nazijua na sitawaangusha hata kidogo,'' alisema huku akishangiliwa.
Alisema kila akiangalia haoni mtu wa kushindana naye na kumshinda katika uchaguzi huo utakaovishirisha vyama vingi vya siasa.
"Mmepoteza nguvu zenu nyingi, muda wenu mwingi, mmetembea umbali
mrefu kuja kunisikiliza, napenda niwahakikishie kwamba CCM itashinda,"
alisema.
Dk. Magufuli jana aligeuka kivutio baada ya kutoa salaam kwa
ufasaha kwa kutumia lugha za kisukuma, kimasai, kichaga, kihehe, kihaya
na kinyakyusa.
SAMIA
Naye mgombea mwenza, Samia, alimpiga kijembe aliyekuwa Naibu Waziri
wa Kazi na Ajira na Mbunge wa Segerea, Dk. Makongoro Mahanga
aliyejiunga na Chadema wiki hii.
Wengine waliojiunga na Chadema ni pamoja na Mbunge wa Kahama, James
Lembeli, Godluck Ole Madeye (Arumeru Mashariki), Ester Bulaya (Viti
Maalum) na aliyekuwa Mwenyekiti wa Wenyeviti wa CCM wa Mikoa na Mkoa wa
Singida, Mgana Msindai.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni