
Katuni.
Kazi ya kuandikisha wapigakura kwa mfumo wa BVR ilianza Februari 23, mwaka huu mkoani Njombe.
Safari ya Nec iliyoanza Februari mwaka huu ilikuwa ni kuandikisha
watu milioni 24 katika mikoa 31 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili
wapate fursa ya kuchagua madiwani, wabunge na rais katika uchaguzi mkuu
unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Tunaipongeza Nec kwa kuhimitisha kazi hii nzito na muhimu katika
kuhakikisha kwamba wananchi wanatumia haki yao ya kidemokrasia
kuwachagua viongozi wao kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Kila
tukitazama nyuma, tunakumbuka changamoto nyingi ambazo Nec ilikumbana
nazo. Hizi ni pamoja na kuanza kazi hiyo kwa kusuasua kutokana na uhaba
wa BVR. Itakumbukwa kwamba awali Nec ilikuwa na BVR 250 ambazo zilikuwa
zimenunuliwa wakati wa kazi ya uandishaji wa majaribio mwaka jana. Hadi
kazi hii inamalizika jana, Nec ilikuwa na BVR 8,000 na zilisambazwa
nchini kote, mkoa kwa mkoa. Ni jambo la kufurahi kwamba sasa kazi hiyo
imekamilika.
Taarifa ambazo Nec imekuwa ikitoa kwenye mikoa mbalimbali ambako
kazi hiyo ilikamilika, zinaonyesha kwamba mwitikio wa wananchi ulikuwa
wa juu sana katika kujiandikisha. Kuna maeneo malengo yalivukwa kwa
zaidi ya asilimia 100. Kazi nyingi nzuri zilifanyika. Sisi tunapongeza
Nec kufikia mwisho huu mwema.
Hata hivyo, tungependa Nec iongeze uwazi na ushirikishwaji wa
wananchi na wadau wote wa uchaguzi, kujua kiuhalisia ni watu wangapi
wameandikishwa, orodha zitolewe kwa wakati jimbo kwa jimbo. Uwazi ndiyo
jambo muhimu katika kufanikisha kazi hiyo. Nia ni kuepuka malalamiko na
hata uwezekano wa kuwa chanzo cha vurugu kwenye uchaguzi.
Tunajua kwa hali ilivyo, itakuwa ni vigumu kuwa na muda wa kuhakiki
daftari la wapigakura kwa maana ya kubandika majina yote ya
waliojiandikisha katika vituo vya kujiandikisha kwa sababu ya muda.
Ni jambo la bahati mbaya kwamba Nec imejikuta katika ratiba
iliyobana sana ya kuandaa uchaguzi mkuu mwaka huu. Inajulikana dhahiri
dhahiri kwamba uchaguzi ni mchakato, siyo upigaji kura pekee yake.
Uchaguzi huanza kwa uandikishaji wapigakura, uteuzi wa wagombea,
ufanyaji wa kampeni, upigaji kura na kuzihesabu kwa uwazi na mwisho
kutangaza matokeo. Huo ni utaratibu wa kisheria. Ni lazima uzingatiwe na
kufuatwa pasi na kisingizio chochote.
Ni imani yetu kwamba Nec itaendelea kujibidiisha kuhakikisha kwamba
hatua zinazofuata katika mchakato wa uchaguzi zinafanyika sawa sawa ili
kujenga imani kwa wananchi kwamba weledi unawaongoza katika kazi hii
muhimu ya kuhakikisha kwamba taifa hili linapata viongozi wanaotokana na
ridhaa ya wananchi.
Tunajua kuwa hatua zilizobakia sasa kwa maana ya kuteua wagombea,
kufanya kampeni, kupigakura na kuzihesabu na mwishowe kutangaza matokeo,
ni muhimu sana.
Ni kwa kutambua ukweli huo tunaamini kwamba Nec haitaiyumba katika
kazi hii, itazingatia weledi, sheria na kanuni zote ili kufikisha mwisho
mwema uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Kadhalika, tunaelewa kwamba hamasa walioyokuwa nayo wananchi
kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ni ishara ya kutambua haki zao na
hivyo kuzitumia vilivyo ili ifikapo Oktoba 25, mwaka huu watumie
vitambulisho walivyopata kuwachagua viongozi wao kwa njia ya
kidemokrasia.
Tunawashauri na kwa kweli kuwachagiza, kwamba kujiandikisha ni
jambo moja, lakini kupiga kura ni jambo la pili. Ni kwa jinsi hii
tunawasisitiza wananchi kuwa watunze vema vitambulisho vyao vya kura ili
wavitumie vema Oktoba 25, mwaka huu kufanya maamuzi juu ya nani
anastahili kuwa diwani, mbunge na rais ili kuwaongoza kwa kipindi cha
miaka mitano ijayo.
Haitakuwa jambo la kufurahi kama kujitokeza kwa wingi kiasi hicho
kwa wananchi nia kuu ilikuwa ni kupata vitambulisho tu. Itakuwa ni jambo
la faraja, la kuenziwa na linalojenga demokrasia na ushiriki mzuri wa
wananchi katika kuamua mustakabali wa nchi yao kama watajitokeza kwa
wingi kwa kasi na kiwango hicho hicho kupiga kura Oktoba 25, mwaka huu.
Tunawaomba wananchi watunze vitambulisho vyao na Oktoba 25, mwaka
huu wavitumie kuamua nani awe diwani, mbunge na rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha 2015-2020.
CHANZO:
NIPASHE
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni