
Shirika la Umeme nchini (Tanesco), juzi lilitangazia umma kwamba nchi nzima itakuwa gizani kwa takriban wiki nzima kuanzia jana.
Shirika hilo lilieleza kuwa hali hiyo inatokana na kuzimwa kwa
mitambo ya gesi inayozalisha umeme kutoka Songosongo mkoani Lindi.
Tanesco ilifafanua kuwa imechukua hatua hiyo kutokana na kazi ya
kuunganisha bomba la gesi kutoka Mtwara na mtambo wa umeme wa Kinyerezi
II.
Aidha, hali ya umeme ilitarajiwa kuwa mbaya zaidi jana kwa kuwa
mitambo yote ya kuzalisha nishati hiyo ilikuwa inatarajiwa kuzimwa ili
kufanikisha kazi hiyo.
Tunaamini kwamba dhamira ya Tanesco ni njema na imelenga kuboresha
utoaji huduma umeme nchini ambayo kwa miaka nenda rudi, imekuwa haikidhi
matarajio ya wateja wake na Watanzania kwa ujumla.
Hata hivyo, sisi hatuamini kuwa hatua ya Tanesco ya kuunganisha
bomba la gesi kutoka mkoani Mtwara na mitambo yake, imekuwa ni ya
dharura kiasi cha kulazimika kutoa taarifa kwa umma siku moja kabla.
Tunasema na tuna imani kwamba mpango wa shirika hilo wa kuunganisha
bomba hilo na mitambo ya Kinyerezi, haukuibuka ghafla tu juzi na hivyo
kulazimika kuwapa wateja wake notisi ya muda mfupi, bali lilijipanga kwa
kwa muda mrefu kwa kazi hiyo pasipo kukurupuka.
Kwa msingi huo, menejimenti ya Tanesco ilipaswa kutoa tahadhari
mapema kwa wateja wake juu ya kuwapo kwa hatua ya kuzima mitambo yake
ili kuwawezesha kujipanga kukabiliana na tatizo hilo.
Ni dhahiri kwamba mamilioni ya watu nchini, hutegemea nishati ya
umeme kwa shughuli mbalimbali za kila siku za kujiongezea kipato pamoja
na viwanda.
Mathalani, ukiachilia mbali viwanda ambavyo kwa asilimia kubwa
hutegemea umeme wa Tanesco, lakini pia wajasiriamali mbalimbali
hutegemea nishati ya umeme kuendeshea shughuli zao za kiuchumi kama vile
saluni za kike na kiume, inateneti, gereji za magari, wauzaji wa
vinywaji baridi na vikali, wauza samaki na nyama, mama ntilie,
wachomeleaji vyuma; kutaja baadhi.
Kwa msingi huo, ni jambo lililo wazi kwamba hatua hii ya Tanesco
kwa kiasi kikubwa itaathiri shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii
ambazo kwa kiasi kikubwa zinategemea nishati ya umeme.
Ni kutokana na hilo, ndipo tupoona umuhimu wa Tanesco ingepaswa
kutoa taarifa ya kukosekana kwa umeme mapema zaidi ili makundi hayo yote
yajiandae vya kutosha.
Kimsingi, Tanesco haikuwatendea haki wateja wake na umma wa
Watanzania kwa kufanya uamuzi huo wa ghafla wa kuzima mitambo yake bila
kujali athari watakazokumbana nazo.
Aidha, hatua hii ya Tanesco kwa kiasi kikubwa pia itaathiri
uzalishaji wa viwandani kwani vitalazimika kuingia gharama za kutumia
majenereta yanayotumia mafuta.
Matumizi ya jenereta, ni wazi kwamba yatachangia kwa kiasi kikubwa
kupandisha bei ya bidhaa zinazozalishwa viwandani na hivyo kuongeza
ugumu wa maisha kwa wananchi.
Viwanda vingi vinaendeshwa kwa bajeti na hatua hii ya Tanesco kuzima ghafla mitambo yake, italeta athari kubwa.
Mbali na shughuli hizo za kiuchumi, lakini pia kuna masuala ya
kijamii kama shughuli za hospitali kwani kwa hatua hii ya Tanesco, ni
dhahiri wagonjwa wengi wanaohitaji huduma za matibabu wataathirika.
Ikumbukwe kuwa Tanzania kwa sasa inapigania kupeleka watu wake
kwenye uchumi wa kati, na kwa msingi huo suala la nishati ya umeme, ni
muhimu kwa watu wa kipato cha chini wanaotaka kuinua hali zao za maisha.
Kwa hakika Tanesco inapaswa kukubali kwamba haikuwatendea haki wateja wake na umma wa Watanzania kwa hatua yake hii.
Hata hivyo, sisi hatupingi dhamira njema ya Tanesco kuboresha
miundombinu ya umeme nchini, tunachosisitiza ni kwmaba yalipaswa kuwapo
mawasiliano bora na ya mapema ambayo yangesaidia wananchi kujipanga
vizuri na athari za makali ya kukatwa kwa umeme.
SOURCE:
NIPASHE
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni