
Mchungaji huyu anazungumza na Nipashe na kugusia baadhi ya mambo ya kukwepa ili kuepusha athari zaidi.
KUKASHIFU KANISA
Kama kiongozi wa kanisa anaelezea kukerwa na baadhi ya wanasiasa
wanaosukuma tuhuma kwa viongozi wa dini wakiwahusisha na rushwa.
Mathalani kudai kuwa maaskofu wamehongwa kati ya Shilingi milioni
60 hadi 300 ili kumkubali mgombea mmojawapo, ni mambo yanayowafanya
waumini kuwafikiria vibaya viongozi wao.
Anasema mbali na rushwa wapo baadhi ya wagombea na hata viongozi
ndani ya jamii wanaohubiri siasa za chuki kuwa baadhi ya makabila ya
Tanzania hawafai kuwa rais wa nchi hii.Kadhalika anasikitishwa na
wagombea wanaodai kuwa upinzani unasababisha uvunjifu wa amani na hata
kutumia mifano ya machafuko katika baadhi ya nchi za Afrika kuwa
ziliamua kuua viongozi wao na sasa raia hao wanahangaika.
Anawataka Watanzania kufahamu kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi.
“Nataka kusisitiza kwa wanasiasa na Watanzania kwa ujumla wetu kuwa yapo
maisha kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa mwezi ujao.
“Ili amani yetu iendelee ni lazima tuache uongo, udini, utaifa wa
kujibagua kwa mfano ‘ubara au uzanzibari’ hata ukanda kwani hiyo ndiyo
mitaji ya kuangamiza taifa na wala siyo kuwa na wanachama wa upinzani.”
Anasema upinzani ni jicho la ziada la kukosoana na upo kikatiba na
si mtaji wa kuvunja amani kama inavyodaiwa na baadhi ya wanasiasa.
“Nawashauri wanasiasa kuwa upendo, amani , haki na wajibu wa kila mtu
katika kutunza umoja ziwe kauli zenu.”
‘UONGO NI MATUSI’
Askofu Mwamalanga akizungumzia madai ya kuzuliana kama kupewa hongo
na kusingiziana anasema kauli za uongo hazina tofauti na hotuba za
matusi au kukashifu kwani zinahamasisha hasira ndani ya jamii hivyo kuwa
chanzo cha vurugu na kuzalisha mitandao ya uovu jambo ambalo ni hatari
kwa vile linatoa mwanya kwa maadui wa ndani na nje kujipenyeza na
kuhatarisha umoja na amani ya nchi.
UVUMILIVU WA LOWASSA
Askofu Mwamalanga anamtaja mgombea wa urais kupitia umoja wa vyama
vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD Edward Lowassa, kuwa mfano wa
uvumilivu wa kuigwa kwani pamoja na kuporomoshewa matusi, kulaumiwa na
watu wengi kwenye kampeni amekuwa mtulivu na mwenye kulenga ujumbe
anaotaka kuuwasilisha kwa wapiga kura.
Badala ya kutumia majukwaa kujibu matusi Lowassa amekuwa mtulivu na
kutaka wale wenye ushahidi wauwasilishe, hivyo wanasiasa wengine
wajifunze na huo ndiyo ustarabu wa kisiasa.
“Nawaomba wanasiasa muigeni Lowassa anafahamu kuwa kuna maisha kabla na baada ya uchaguzi.”
“Napendekeza baada ya uchaguzi mkuu itolewe tunzo ya utulivu au
heshima wakati wa kampeni. Naamini kwamba hii itasaidia wagombea na
wapambe wao kuwa watulivu wakati wote wa kampeni na baada ya uchaguzi
Mkuu ili kulinda amani na utlivu wa nchi.”
VYOMBO VYA ULINZI
Anapozungumzia ‘jeuri’ ya Dk Wilbroad Slaa, kuwa analindwa na
maofisa wa usalama wa taifa, anaona kuwa si jambo la kutamba kwa vile
linatoa nafasi kwa watu kuwaza na hata kuzua mambo mengine ambayo
hayaleti amani.
Anasema vyombo vya umma kama Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec),
Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) na majeshi mengine
yalinde umma siyo mtu binafsi.
Vyombo hivi ni muhimu katika kusimamia haki na kuendelea
kuwakumbusha wanasiasa na Watanzania kuhusu uchaguzi huku vikibeba
jukumu la kuufanya umma uwe wa utulivu na amani kwa ustawi wa taifa.
Anaamini kiongozi wa siasa kutukana na kutoa tuhuma nyingi lakini
pia akilindwa si jambo jema. Anawakumbusha Takukuru kuyafanyia kazi
madai kuwa kuna rushwa imetolewa kwa vile Slaa anaweza kuwa ushahidi na
kutibitisha au kukanusha tuhuma hizo.
Anaielezea hatua ya kuwatukana maaskofu kama kuporomoka kwa maadili
kwani kumeambatana na matusi ,uongo na masingizio kuwa zaidi ya
maaskofu 30 kati ya 34 wa Kanisa Katoliki wamehongwa kiasi kikubwa cha
fedha.
Yapo maelezo mengine kuwa viongozi wa madhehebu mengine wamepewa
rushwa na Askofu Josephat Gwajima, anaunganishwa na rushwa jambo ambalo
lina lenga kuchafua kanisa na waumini.
“Hali ya kuporoka maadili ndani ya jamii na heshima kushuka
miongoni mwa baadhi ya wanasiasa kunanilazimisha kukumbushana kuwa kuna
maisha na urafiki baada ya uchaguzi mkuu wa mwezi ujao hivyo tunapaswa
kuchunga kauli za vinywa vyetu ili kuepusha kuwa na maadui wa kisiasa na
hata wa maisha yetu.”
Anaeleza kuwa kusema uongo dhidi ya watu fulani kunaweza kujenga
uadui na kuhamasisha hasira ndani ya jamii hivyo kuwa chanzo cha vurugu
na visasi si baina ya watu lakini hata miongoni mwa wanasiasa.
Anasisitiza kuwa kila jambo linaloonekana mbegu yake ni ‘mawazo’
ambayo huwa ‘maneno’, hivyo kuchunga ulimi ni jambo muhimu kuliko
kingene chochote kwa kuwa kauli jambo linatokea.
CHANZO:
NIPASHE
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni