WAJIBU wa kila mzazi nchini mwenye mtoto aliyefikisha umri wa kwenda shule ni kuhakikisha mtoto huyo anakuwa darasani, lakini bado wapo wazazi wanaoshindwa kutekeleza wajibu huo.
Achilia mbali watoto wanaozurura mitaani kutokana na kukosa nafasi ya kwenda shule, lakini wapo pia watoto wanaoishi na wazazi wao lakini hawakupata wasaa wa kukaa darasani na kumsikiliza mwalimu kutokana na maisha duni ya wazazi wao.
Hata hivyo, ieleweke Tanzania ya sasa si ile ya zamani ambapo idadi ya wasomi ilikuwa ndogo kwa sababu serikali haikuwa na shule za kutosha.
Serikali imejaribu kufuta ada na kuongeza idadi ya shule, walimu wanapewa nafasi kubwa kusomeshwa kwa mikopo vyuoni pamoja na kuhangaikia kuweka sawa maslahi yao wanapoanza kazi.
Yote hiyo ni kutaka kufanya elimu ni suala la lazima, na atakayeshindwa kutimiza wajibu huo achukuliwe hatua bila kuonewa.
Kutoa ni moyo usambe ni utajiri, walishasema wahenga. Wapo baadhi ya waungwana wanaowiwa kutoa msaada kwa wasiojiweza ili kila Mtanzania afikishe lengo la kupata elimu mbali ya hali ngumu ya maisha.
Geofrey Ngunya ni mkuu wa kituo cha Mwalimu Education Center mkoani Morogoro, kituo kinatoa elimu kwa wanafunzi wanaotoka katika kaya masikini ikiwa ni pamoja na watoto wanaoishi katika mazingira magumu mitaani.
Asilimia kubwa ya wanafunzi wana umri mkubwa, zamani wanafunzi wa aina hiyo waliona aibu kukaa na watoto waliowapita umri kwa miaka mingi.
Kwa kuwa majuto ni mjukuu watu kama hakuna mwenye kujisikia vibaya, kila mmoja anafurahia maisha kwa kuwa elimu haina mwisho na kimbilio la maisha ni elimu.
Hata hivyo, kituo hiki bado kinahitaji watu wenye uwezo na moyo wa kujitolea kufikiria namna ya kuwasaidia wanafunzi wanaojiunga kupata elimu. Kwa sababu gharama wanazotozwa ni ndogo ingawa kuna gharama nyingine zinazohitajika kutolewa na wasamaria wema.
Kituo hiki kilianzishwa mwaka jana, lengo ni kutoa fursa kwa watu waliokosa nafasi ya kujiendeleza kielimu kwa sababu mbalimbali ikiwemo hali ngumu ya uchumi na kutoka katika familia zilizodharau elimu.
Mwalimu Ngunya anaeleza kuwa Watanzania wengi hasa katika kipindi hiki cha utandawazi wanatamani kupata elimu, lakini wanashindwa kufikia lengo, hilo lilimsukuma kutaka kuwasaidia kwa kutumia uwezo aliojaliwa na Mungu.
“Wapo watu wanaotamani kupata elimu ili wafunguke macho, lakini wanashindwa kutokana na mazingira ya kiuchumi. Sisi tuliobahatika tunawasaidia vipi, fahamu serikali haiwezi kufanya kila kitu tunahitaji kuwasaidia.
“Ndipo nilipopata wazo la kuanzisha shule ili kurudisha nilichokipata katika jamii, naweza kusema wazazi wangu wamenilipia ada ndio maana nikasoma lakini jamii nayo imenisomesha kwa kuyajua mengi ambayo wazazi wangu tu wasingeweza,” alisema Ngunya.
Anaeleza jina la kituo chake linafahamika zaidi kama “Mwalimu” kwa kuwa yeye ni mwalimu kitaaluma, ameamu kuisaidia jamii kwa kutoa elimu bure kwa wasiojiweza, wale wanaojiweza wanalipia gharama kidogo.
Anafafanua kuwa, maendeleo ya kitaaluma hususani kwa watoto wanatoka katika familia duni ni mazuri ukilinganisha na familia zenye uwezo, hali hiyoo inampa hamasa ya kuendelea kutoa msaada kwa wanafunzi wenye hali ngumu kwnai wanaonekana wanataka kuelimika kwa namna yoyote ile.
Anaeleza kwa kwa kuwa mwitikio wa watu ni mkubwa anatazamia kupanua kituo ili vyumba vya madarasa viongezeke, furasa ipo kikubwa ni kuchukua hatua ndio maana anawakaribisha wale wote waliokosa elimu kutokana na umasikini.
Alipoulizwa anajuaje hali za wanafunzi wanaokuja kuoba msaada wa kusomeshwa bure, mwalimu huyo alisema “Unajua hapa tunafanya kazi ya Mungu, hivyo utaratibu tunaoutumia ni kuwataka wale wote wanaohitaji kusaidiwa kujaza fomu na kupata wadhamini watakaokiri ni kweli wanaishi katika mazingira magumu na wanahitaji msaada wa kweli.
“Mbona hata katika vyuo vikuu mikopo imelenga wale wasiojiweza lakini hawaweki masharti magumu ili ujulikane familia yako ni duni wanakuacha ujieleze.”
Anasisitiza kuwa taifa lolote lililoendelea kiuchumi ukichunguza utabaini limewekeza katika elimu, kwa sababu elimu ndiyo siri ya mafanikio katika nyanja zote. Yeye kujitolea kutoa elimu bure anaamini ipo siku taifa litanufaika kupitia kwake kwani hakuna ajuaye kesho itakuaje.
Kwa upande wao wanafunzi wanaeleza kuwa wanamshukuru sana Mungu kwa msaada walioupata, kwani walikuwa wanatamani sana kupata elimu kama walivyo watu wengine lakini walishindwa kufanya hivyo kutokana na mazingira wanayoishi kutoruhusu kufanya hivyo.
Imeandikwa na WARIOBA IGOMBE
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni